Image
PhotobyMarceloSchneider_2021_03_02_21.jpg

Kutoa chanjo kwa wingi huleta matumaini katika nyakati za kutisha.

Photo:

na Claus Grue *

Wakati ueneaji wa virusi vya korona unakaribia kudhibitiwa, changamoto zinabaki katika nchi ambapo janga hilo linahafifishwa, au hata linakanushwa. Uvumi na nadharia za kubuni za kila aina kuhusu mipango ya chanjo zinawazuia watu kuamua kupewa chanjo.

"Habari za upotoshaji kama hizo zinaonyesha tu vile ilivyo muhimu kuratibu jitihada kati ya sekta ya afya na mashirika ya kidini, na kuzingatia masuala ya kiroho wakati wa kuzindua operesheni kubwa za tiba," Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mch. Prof. Dk. Iona Sauca, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa la Ulimwengu, alipotoa taarifa kwa umma kuwahimiza viongozi wa dini kujenga imani, kupambana na habari potofu na kuchangia maamuzi yanayokubaliwa katika muktadha wao.

Kuhusianisha masuala ya kitabibu na kiroho

Kusita kupokea chanjo kwa kiasi fulani pia ni changamoto katika nchi ambapo mambo yanachukuliwa kwa uzito na chanjo inahimizwa. Wataalamu wa tiba na maafisa wa serikali wametoa wito kwa watu kupokea chanjo pale inapotolewa, kwa sababu inaokoa maisha na hupunguza mzigo kwenye hospitali na vituo vingine vya huduma za afya. Lakini, kama ambavyo viongozi wa kanisa wanavyosisitiza mara nyingi, pia kuna mwelekeo wa kiroho kwa janga hilo, ambapo harakati ya kiekumene inaweza kuleta mabadiliko, na ambapo WCC na mashirika mengine ya kidini yanatekeleza wajibu muhimu kwa mshikamano ili kuhamasisha watu kukubali chanjo, vile vile kuondoa uvumi na nadharia potofu zisizo na msingi.

Kote ulimwenguni, mabaraza ya kitaifa ya makanisa na jamii za kidini hufanya kazi pamoja na mashirika ya afya kupinga habari za uwongo na kuhakikisha kuwa masuala ya kitabibu na kiroho yanahusianishwa vizuri.

"Hatuwezi kusimama bila kufanya kazi wakati watu wanateseka na wanazuiliwa kupokea chanjo ambazo tayari zipo kwa ajili yao. Hili halishusu tu kuwalinda watu dhidi ya kuugua sana, na wakati mwingine kufa, ni kuhusu mshikamano na huruma, ” Sauca anaendelea.

Hivi karibuni WCC iliungana na mashirika ya afya ya Kikristo zaidi ya 30 ulimwenguni kote katika kuibua dukuduku juu ya kutokuwepo usawa katika upatikanaji wa huduma za afya na chanjo za COVID-19. Katika taarifa, mashirika hayo yanawahimiza viongozi wote wa serikali kufanya kila kitu kulingana na uwezo wao ili kufanya chanjo za COVID-19 kuwa jambo jema la umma la kiulimwengu - zipatikane na zigawanywe kwa usawa.

Mnamo Machi 15, yalifanyika mafunzo kwa njia ya mtandao yaliyoandaliwa na WCC ili kuangalia namna makanisa yanavyoweza kuhakikisha kuwa watu wasio na utaifa hawaachwi nyuma katika mipango ya kitaifa ya utoaji wa chanjo ya COVID-19.

Kushughulikia hali ya kusita kupokea chanjo

Kuunga mkono taarifa za kisayansi katika muktadha wa kiimani ni njia nyingine ya kuifikia jamii ambapo watu kwa sababu mbalimbali husita kukubali chanjo. Mwezi Februari, Mkutano wa Makanisa ya Ulaya uliandaa mafunzo kwa njia ya mtandao, uliokuwa na kichwa cha habari "Chanjo - laana au baraka? Mtazamo wa kiroho na kitheolojia kuhusu chanjo ya COVID-19,”Ambapo wataalamu wa tiba na wanatheolojia walichunguza hali ya sasa ya maarifa ya kisayansi kuhusu chanjo ya COVID-19 kutokana na mtazamo wa maadili ya Kikristo. Mafunzo hayo, ambayo yalichagizwa na wasilisho la majadiliano, yalitoa vidokezi na taarifa zilizojikita kwenye ukweli kwa makanisa na jamii, yakishughulikia masuala ya kusitasita na nadharia potofu.

Katika Mashariki ya Kati, ambapo janga hili bado ni changamoto nyingine pamoja na chagamoto kadhaa, Baraza la Makanisa la Mashariki ya Kati limekuwa likitoa kipaumbele kwa habari mpya zenye ukweli katika tovuti yake, nchi kwa nchi, kuhusu hali ilivyo wakati huo kwa kuangalia idadi ya visa, idadi ya waliopona na idadi ya vifo. Viongozi wa kanisa wanawahimiza watu kupata chanjo, ingawa upungufu wa chanjo umesababisha ucheleweshaji.

Kuongoza kwa mfano

Katika mojawapo ya nchi zilizoathirika zaidi, Marekani, ambapo zaidi ya watu nusu milioni wamekufa kwa COVID-19 hadi sasa, Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kristo linahimiza chanjo kupitia tovuti ya "Faith4Vaccines", nyenzo inayotengenezwa kwa ajili ya viongozi wa dini ambapo visa kuhusu chanjo vinaweza kutolewa na kuenezwa zaidi kupitia mitandao ya kijamii. Baraza pia linashiriki katika kampeni ya mtandaoni ya “#pastors4vaccines pledge,”, ikihimiza watu kupata chanjo na kuilinda jamii yao.

"Bado tunaamini kwamba ikiwa watu wanashuhudia watu wanaowaamini wamepewa chanjo na kuwahimiza kufanya hivyo, watasikiliza. Kwa hivyo, kampeni yoyote inahitaji kuwashirikisha viongozi wanaoaminika wakitoa ujumbe. Elvis Presley aliwahi kutumiwa ili kuwafanya watu wapokee chanjo ya polio. Tunawahimiza maaskofu na viongozi wa usharika kushiriki picha zao za chanjo, ”anasema Cynthia Griffiths, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Maendeleo katika Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kristo.

Wito wa namna hiyo pia utaungwa mkono wakati wa Wiki ya Maombi ya WCC wakati wa COVID-19, mpango wa tarehe 22 - 27 Machi, katika kujibu maombi kutoka kwa makanisa washirika na washirika wa kiekumene. Kwa wiki nzima, sala na nyenzo za kiroho zinazozalishwa ili kukabiliana na janga hilo zitatolewa. Siku ya tano ya sala, iliyo na mada ya "ulinzi", hali ya kusitasita kupokea chanjo inayosababishwa na habari potofu itashughulikiwa. Viongozi wa kidini na wa kiroho wanahimizwa kuongoza kwa mfano kwa kupata chanjo hadharani ili kuamsha ujasiri na kuthibitishia jumuiya zao kuhusu chanjo husika.

"Ikiwa watu wa dini na jumuiya ya huduma za afya watazungumza kwa sauti moja, itachangia sana kushinda hali ya kutokuwa na imani na upinzani," Sauca anaamini hivyo..

Wasiwasi mkubwa nchini Brazil na Tanzania



 Brazil na Tanzania ni mifano miwili ya nchi ambazo janga hilo limekuwa halichukuliwi kwa uzito. Nchini Brazil, viwango vya maambukizi na vifo vimekuwa vikiongezeka sana na nchi inapambana ili kudhibiti mlipuko huo. Baraza la Maaskofu la Maaskofu wa Kanisa la Anglikana Brazil limetoa waraka wa kichungaji katikati ya hali mbaya ya ugonjwa wa COVID-19: "Wimbi kubwa la maambukizi na aina mpya ya virusi imeleta maumivu zaidi na zaidi, uchungu na hisia kwamba tupo katika upepo wa kisulisuli ambamo ni neema ya Mungu tu ndiyo inatumika kama ngao," inasema sehemu ya waraka huo.Maaskofu pia wanasema kwamba ucheleweshaji wa majibu ya mamlaka ya serikali umesababisha "kutotoa ushirikiano" kwa upande wa umma.

“Brazil inakaribia sana kutengwa na mataifa mengine duniani. Ili kurekebisha hali hii hatua ya haraka lazima ichukuliwe kujitenga, kuendelea kutekeleza shughuli muhimu tu na kutoa chanjo kwa wote" sehemu ya waraka huo inasomeka hivyo.

Nchini Tanzania, hayati rais John Pombe Magufuli, ambaye kifo chake kilitangazwa jana na serikali ya Tanzania, alikanusha kuenea kwa virusi hivyo na akakataa kununua chanjo kwa ajili ya watu wake. Sasa kuna wasiwasi unaoongezeka juu ya wingi wa visa vya maambukizi nchini Tanzania.

Katika nchi jirani za Kenya na Zambia, msimamo juu ya chanjo bado umegewanyika na umma umeachwa katika wasiwasi bila kuwa na uhakika kama watapata chanjo au la. Muungano wa Makanisa Afrika yote umetoa arifa ya maombi katika kuunga mkono mpango wa chanjo barani humo, na kuhimiza maombi ya ulinganifu kati ya sayansi na imani, kwa sababu zote zinaaminika kuwa na jukumu muhimu katika kukabiliana na tatizo hilo. Maombi kwa ajili ya mpango huo kufanikiwa, na kwamba Afrika ipate vifaa stahiki na vya kutosha vya chanjo inazohitaji ili kumaliza janga hilo, pia zinaombwa katika arifa hiyo.

Harakati ya kiekumene na ushirika wake wa makanisa upo katika nafasi nzuri ya kuwafikia watu, hasa katika maeneo ya mashambani, kwa kuwapa habari ya kweli, inayojikita kwenye imani kuhusu umuhimu wa kupokea chanjo.

"Ni jukumu letu kufanya kila tuwezalo ili kuleta tumaini, kupunguza mateso katika jamii zilizoathirika na kupunguza mzigo kwa wafanyakazi wa huduma ya afya waliochoka. Kukabiliana na habari za uwongo na nadharia potofu ni sehemu ya kazi hiyo, ”anahitimisha Sauca.

* Claus Grue ni msadi wa mawasiliano wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

As COVID-19 vaccines roll out, WCC urges religious leaders to combat misinformation (Wakati chanjo ya COVID-19 inatolewa, WCC inawahimiza viongozi wa dini kupambana na habari potofu) - Taarifa kwa umma ya WCC iliyotolewa Februari 24 mwaka 2021

Nyenzo za COVID-19 za WCC